Tuesday, August 7, 2012

OKWI AMUACHA KWENYE MATAA BIN KLEB, AREJEA SIMBA, YUPO SIGARA HIVI SASA.

 Okwi wa pii kutoka kulia. Wa kwanza ni Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geoffrey Nyange 'Kaburu'. na Kulia kabisa ni Katibu wa Simba, Evodius Mtawala

 Emmanuel Okwi amemtoroka Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Abdallah Ahmad Bin Kleb aliyemfuata Kampala, Uganda na kurejea Dar es Salaam kujiunga na klabu yake, Simba SC.
Okwi ametua leo Dar es Salaam na sasa hivi yupo Uwanja wa Sigara, Chang’ombe kwenye mazoezi ya klabu yake.

Jana Yanga inadaiwa walianza mazungumzo na mshambuliaji huyo wa Simba SC, na vyanzo vinasema ameomba mshahara wa dola za Kimarekani 3,000 kwa mwezi ili asaini klabu hiyo, ingawa haijulikani kuhusu mkataba wake wa sasa na klabu yake, Simba SC.
Bin Kleb alizungumza na BIN ZUBEIRY kutoka Kampala jana na kusema; “Ndio, nipo Uganda, nipo Kampala hivi sasa, nakubali Rage (Ismail Aden, Mwenyekiti wa Simba), alinizidi maarifa Kigali (Rwanda) katika usajili wa Mbuyu Twite, ila sasa na mimi nataka kulipa kisasi, we subiri tu muda si mrefu utapata habari,”alisema Bin Kleb.
Hili linakuwa bao la tatu, Simba wanaipiga Yanga ndani ya wiki mbili, kwanza saini ya Mrisho Ngassa kutoka Azam FC, baadaye Twite na sasa Okwi.
Okwi amerejea wiki iliyopita Uganda, baada ya takriban wiki tatu za kuwa majaribio katika klabu ya FC Red Bull Salzburg ya Wals-Siezenheim, Austria ambayo hivyo haitamnunua.
Simba ilikuwa ina matumaini ya kupata Euro 600,000 ambazo klabu hiyo, ilikuwa tayari kutoa iwapo Mganda huyo angefuzu majaribio.
Awali, Simba ilipata ofa ya kumuuza Okwi kwa Sh. Bilioni 2 kwa klabu ya Mamelodi Sundown ya Afrika Kusini, lakini mshambuliaji huyo akasema anataka kwenda Ulaya.
Awali Olando Pirates ya Afrika Kusini ilimuomba Okwi akafanye majaribio huko kama angefuzu wangemsajili dau la dola 550,000 kabla ya kuibuka kwa taarifa za kutakiwa Italia na klabu ya Parma.

No comments: