Okwi.
Baada ya kuwepo kwa tetesi za Yanga kutaka kumsajili mshambuliaji wa kimataifa wa Simba, Emmanuel Okwi, hatimaye ameongezewa mkataba wa miaka miwili kwa dau la sh milioni 50 pamoja na gari la kifahari.
Hivi karibuni, nyota huyo ambaye alikuwa nchini Austria kwa ajili ya majaribio ya kucheza soka ya kulipwa katika klabu ya Red Bull Salzburg kabla ya kurejea nchini Jumanne, amekuwa akidaiwa kuwaniwa na Yanga.
Hivi karibuni, nyota huyo ambaye alikuwa nchini Austria kwa ajili ya majaribio ya kucheza soka ya kulipwa katika klabu ya Red Bull Salzburg kabla ya kurejea nchini Jumanne, amekuwa akidaiwa kuwaniwa na Yanga.
Chanzo cha habari kutoka ndani ya Simba kinaeleza kwamba, zoezi hilo lilifanyika juzi likiendeshwa na wajumbe wawili wa Kamati ya Usajili, ambao walitoa kiasi hicho cha fedha ili kumbakiza, Okwi Msimbazi.
Imeelezwa kuwa Simba wameona wamuongeze mkataba Okwi, ili kumuepusha na mpango uliokuwa ukifanywa na mahasimu wao nchini, Yanga kutaka kumsajili.
“Tayari tumeshamfunga Okwi kwa sasa, hivyo mahasimu wetu walie tu, tumempa miaka miwili kwa dau la mil. 50, pia tumempa gari na mambo mengine madogomadogo tumeyaweka sawa,” alisema mtoa habari huyo.
Nyota huyo, mkataba wake umebakiza miezi minne kabla kumalizika ambapo kuna taarifa kwamba aliwataka viongozi wa Yanga wampe sh milioni 56 ili aweze kumwaga wino Jangwani.
Katika hatua nyingine, Simba jana ilihitimisha Wiki ya Simba na Jamii kwa kutoa misaada yenye thamani ya sh milioni 1.5 katika kituo cha kulea watoto yatima cha Maunga, kilichoko Kinondoni Hananasif, Dar es Salaam, kwa lengo la kuwafariji.
Katika ziara hiyo, baadhi ya wachezaji waliohudhuria ni pamoja na Okwi, Juma Nyosso, Uhuru Suleiman na wengineo sambamba na baadhi ya viongozi chini ya Makamu Mwenyekiti, Geofrey Nyange ‘Kaburu’, ambaye alisema wameona watembelee kituo hicho, kwani watoto hao pia wanahitaji faraja na kuwa huo ni mwanzo tu watakuwa wakifanya hivyo mara kwa mara.
Wakiwa kituoni hapo, walikabidhi fedha taslimu sh 500,000 pamoja na mahitaji mbalimbali ikiwemo unga, mchele, sabuni na vinginevyo
No comments:
Post a Comment