Taarifa ambazo zimetufikia zinaeleza kuwa, watu 45 wamejeruhiwa na
kukimbizwa hospitalini kufuatua ajali iliyohusisha mabasi matatu ya
abiria katika eneo la Ikundi kwa Makunganya, mpakani mwa Wilaya za
Morogoro na Mvomero, asubuhi ya leo.
Kwa mujibu wa mwandishi mmoja wa habari aliyeongea na Jukwaa Huru kwa
njia ya simu kutokea mjini Morogoro, ajali hiyo imehusisha mabasi ya
Shabiby Video Line, Sumry High Class na Ally’s Coach na kwamba mabasi
yote yamepata ajali katika eneo hilo.
Akifafanua zaidi kuhusu tukio hilo, mwandishi huyo amesema kuwa,
waliokuwa katika eneo la tukio wamewaeleza waandishi kuwa awali, basi la
Shabiby lililokuwa likitokea Dodoma kuelekea Dar es salaam, lilipinduka
kutokana na hali ya hewa kuwa mbaya katika sehemu hiyo, na kufuatiwa na
mabasi hayo mengine mawili ambayo yalikuwa yakitokea Dar es salaam
kuelekea Mwanza.
Ameongeza kuwa, licha ya chanzo cha ajali kutokuwekwa wazi hadi sasa,
upo uwezekano mkubwa kuwa chanzo hicho kikawa ni mwendo kasi ambao
ulisababisha mabasi hayo kukumbwa na mkasa huo, hasa kutokana na ukweli
kuwa eneo hilo ni moja ya maeneo ambayo wataalamu wa barabara wamekuwa
wakilielezea kuwa ni eneo korofi kipindi cha jua kali sana au wakati
mvua zikiwa zinanyesha.
Taarifa zaidi zitawajia pindi vyanzo vyetu vya habari vitakapokuwa vikiziwasilisha.
Aidha, hili ni tukio la tatu la ajali kuripotiwa katika siku ya leo,
baada ya ajali nyingine ambayo imetokea maeneo ya Kibaha na kuhusisha
lori la mafuta lililopinduka na mafuta kumwagika, huku nyingine
ikielezewa kutokea katika eneo la Mto Wami, barabara ya Chalinze Segera
No comments:
Post a Comment