Dk. Ulimboka.
Kutekwa, kupigwa na kuteswa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya
ya Chama cha Madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka na hatimaye kufungiwa kwa
Gazeti la MwanaHalisi kwa muda usiojulikana, kumeleta kizaazaa katika kampuni ya
simu za mkononi ya Tigo, Tanzania Daima Jumatano limebaini.
Habari kutoka ndani ya kampuni hiyo ya simu yenye
mtandao mpana nchini, zinasema kuwa zaidi ya wafanyakazi 30 wamefukuzwa kazi na
wengine wako kwenye uchunguzi wakituhumiwa kuvujisha mawasilino ya siri ya simu
za wateja kwa Gazeti la MwanaHalisi.
Kwa mujibu wa habari hizo, taarifa za mawasiliano za
simu zinazodaiwa kuvujishwa na wafanyakazi hao, zilikuwa kati ya Dk. Ulimboka,
Afisa Usalama wa Ikulu na watu aliowasiliana nao kabla ya kutekwa.
Rais Jakaya Kikwete amepata kuliambia taifa mara mbili
kwa njia ya televisheni, mwishoni mwa Juni na alipozungumza na wahariri wa
vyombo vya habari wiki iliyopita, kwamba serikali yake haihusiki kuteka, kutesa
na kumtupa daktari huyo porini.
Naye Waziri Mkuu Mizengo Pinda amepata kuliambia Bunge
kuwa, serikali yake haihusiki na utekaji, utesaji na kuhoji, “...serikali imteke
ili iweje?”
Hivi karibuni serikali ililifungia Gazeti la
MwanaHalisi baada ya kuandika habari iliyomtaja ofisa mmoja wa Idara ya Usalama
wa Taifa Ikulu (TISS), kuwa ndiye aliyetekeleza mpango wa kumteka, kumpiga na
kumtesa hadi kumjeruhi Dk. Ulimboka, ambaye kwa sasa anaendelea na matibabu
kwenye hospitali moja nchini Afrika Kusini.
Kwa mujibu wa habari hiyo ambayo serikali inadai kuwa
ni ya uchochezi, MwanaHalisi ilianika namba ya simu ya ofisa huyo pamoja na watu
wengine wanaodaiwa kuhusika katika tukio hilo linaloendelea kuchunguzwa na
kamati maalumu iliyoundwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai
(DCI).
Vyanzo vya habari kutoka kwa baadhi ya wafanyakazi
waliokumbwa na sekeseke hilo, zinasema kuwa waliofukuzwa wengi ni wafanyakazi wa
kitengo cha IT ambao wanadaiwa kuhusika kutoa taarifa za siri ya mawasilino kati
ya Dk. Ulimboka na watu wanaoaminika kuwa ni wabaya wake.
Mmoja wa wafanyakazi kutoka Kampuni ya Tigo, aliliambia
gazeti hili kuwa mbali na kutuhumiwa kutoa siri kwa Gazeti la MwanaHalisi,
wafanyakazi wengine wametimuliwa kwa madai ya kufanya udanganyifu kwenye huduma
za Tigo Pesa na kujipatia fedha.
“Kweli watu wengi wamefukuzwa wakituhumiwa kutoa siri
kwa Gazeti la MwanaHalisi, lakini wengine walikuwa wakishirikiana na mawakala wa
Tigo Pesa kuiibia kampuni.
“Kwa mfano mfanyakazi alikuwa anakubaliana na wakala
kumwingizia kiasi kama cha sh milioni moja, lakini anaweza kuingiza hadi sh
milioni 1.5 na kati ya hizo sh 500,000 ni mali yake,” alisema mfanyakazi
huyo.
Akizungumzia na Tanzania Daima Jumatano, Mhariri Mkuu
wa Gazeti la MwanaHalisi, Jabir Idrissa alishangazwa na taarifa za Tigo
kuwafukuza wafanyakazi wake kwa sababu ya habari iliyochapishwa na gazeti
lake.
“Chanzo chetu cha habari hakikutoka kwa wafanyakazi wa
Tigo. Kama wamefukuzwa kwa sababu ya MwanaHalisi, wamewaonea bure. Kama Tigo
ndio waliotupa taarifa na zile za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), zilitoka
wapi?” alihoji Jabir na kusisitiza wafanyakazi hao wameonewa bure.
Ofisa Uhusiano wa Tigo, Edward Shila, alipohojiwa
kuzungumzia tukio hilo, hakukubali wala kukataa madai hayo na kumtaka mwandishi
kumtumia maswali kupitia e-mail yake ili aweze kuyatolea majibu
kiofisi.
“Kama una maswali naomba uniandikie kupitia e-mail
yangu ambayo nakutumia sasa hivi…maana siko tayari kutoa kauli yoyote isiyokuwa
ya kiofisi,” alisema.
Naye Omary Matulla ambaye amejitambulisha kuwa ni ofisa
wa kitengo cha kumbukumbu katika kampuni hiyo, alikanusha kuwapo kwa taarifa za
kufukuzwa wafanyakazi wa kampuni hiyo.
Alisema kuwa kila mfanyakazi ana mipaka ya kufanya kazi
katika kampuni hiyo, na pia ni wajibu wa kila mtumishi kutunza siri
kubwa.
“MwanaHalisi ana mbinu zake za kupata habari wala
haiwezekani kupata habari kupitia kampuni yetu na hata hivyo jambo hilo si
rahisi hata kidogo kutokea,” alikanusha Omary.
Dk. Ulimboka alitekwa usiku wa Juni 26, kusukumizwa
kwenye gari, kupigwa, kufungwa mikono na miguu, kunyofolewa kucha na kutolewa
meno na hatimaye kutupwa katika msitu wa Mabwepande nje kidogo ya Jiji la Dar es
Salaam.
Tangu kutokea kwa tukio la kutekwa kwa Dk. Ulimboka,
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na wanaharakati wa kutetea haki za
binadamu, wamekuwa wakiinyoshea kidole serikali kwamba ndiyo
iliyohusika.
Kamanda wa Kanda Maalumu ya Polisi mkoani Dar es
Salaam, Suleiman Kova, hivi karibuni alitangaza kumfikisha mahakamani mtu mmoja
aliyedai kukiri kuhusika na utekaji wa Dk. Ulimboka.
Kova aliwaambia waandishi wa habari kuwa, polisi
wamekamata mtu aitwaye Joshua Malundi kutoka Kenya ambaye amekiri kumteka na
kumtesa Dk. Ulimboka.
Alidai kuwa mtuhumiwa alikwenda kutubu katika Kanisa la
Ufufuo na Uzima, Kawe, Dar es Salaam.
Lakini hata hivyo, mchungaji wa kanisa hilo, Josephat
Gwajima alikana kauli ya Kova juu ya mtuhumiwa huyo, akisema hajakwenda kutubu
kwao.
Chanzo: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment