Saturday, August 11, 2012

AZAM WAWAACHIA SIMBA NGASSA WAO.

Ngassa.
 Azam FC imeamua kusitisha mpango wa kuwataka kusitisha kumtoa kwa mkopo kwa Mrisho Khalfan Ngassa Simba SC na kumuacha aendelee na maisha mapya Msimbazi, lakini itaendelea kupambana kuhakikisha inapata haki yake juu ya kiungo wake, Ramadhan Chombo ‘Redondo’.
“Huo mpango umekufa, tumegundua haiwezekani, lakini tumejifunza sana, hatuwezi kurudia kosa,”alisema kiongozi mmoja wa Azam FC.

Azam FC tangu juzi usiku ilikuwa inafikiria kusitisha mpango wa kumtoa kwa mkopo katika klabu ya Simba, kiungo wake huyo, Ngassa, kufuatia kitendo cha Wekundu hao wa Msimbazi, kumsajili ‘kibabe’ kiungo wao mwingine, Ramadhan Chombo ‘Redondo’.
“Tunapitia sheria na kanuni za usajili wa mkopo kuona kama tunaweza kufanya hivyo, tukigundua tunaweza, tunawapokonya mchezaji wetu, si watu waungwana hawa, na hatutahitaji tena uhusiano wa aina yoyote na wao, labda klabu ipate viongozi wengine, si hawa wa sasa,”alisema juzi kiongozi mmoja wa Azam.
Azam walimtoa kwa mkopo Ngassa wiki iliyopita, baada ya kukerwa na kitendo cha mchezaji huyo kubusu jezi ya timu yake ya zamani, Yanga, katika Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, dhidi ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Alifanya hivyo, baada ya kufunga bao la ushindi akitokea benchi na kuiwezesha Azam kutinga fainali ya michuano hiyo, ambako walifungwa na Yanga 2-0, naye kwa mara nyingine akitokea benchi na kushindwa kufunga, hivyo kutuhumiwa kucheza kinazi.
Ilielezwa kwamba Simba walitoa Sh. Milioni 25 kumnunua kwa mkopo mchezaji huyo, ingawa baadaye Simba wakasema waliununua mkataba wa mwaka mmoja aliobakiza mchezaji huyo Azam FC, nao wakamuongezea wa mwaka mmoja kwa kumsainisha kwa Sh. Milioni 30, kati ya hizo Milioni 12 akipewa taslimu na 18 akipewa gari.
Inavyoonekana, Redondo aliwadanganya Simba kwamba amemaliza mkataba na Azam, wakaingia mkenge na kumpa Sh. Milioni 30 wakimsainisha mkataba wa miaka miwili, wakati mkataba wake na Azam unamalizika Juni mwakani.
Hili ni kosa sawa na ambalo Simba walilifanya katika usajili mwingine wa mchezaji wa Azam, Ibrahim Rajab ‘Jeba’, miezi mitatu iliyopita ambaye alikuwa kwa mkopo Villa Squad wao wakaenda kumsajili bila kuwasiliana na klabu yake kujua kuhusu mkataba wake, matokeo yake baadaye mchezaji huyo akarejea Azam.
Simba nao wana lalamiko kama hilo, dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga wanaowatuhumu kumsajili beki Kevin Yondan, wakati bado ana makataba na Wekundu hao wa Msimbazi, ingawa TFF iliweka sawa kwa kusema Yondan hakuwa na mkataba na Simba SC.
Baadaye Simba ilitoa ufafanuzi, kwamba ilimuongezea mkataba Yondan baada ya ule wa awali kumalizika na ikawa inasubiri muda wa usajili ufike wauwasilishe TFF. Lakini katika kesi ya awali, Simba walipoupeleka mkataba wao mpya na Yondan, ulionyesha mchezaji huyo anatakiwa kuanza kuutumikia mkataba huo, Desemba mwaka huu, hivyo TFF ikasema kwa wakati ambao yuko huru, aichezee Yanga.
Sakata la Yondan litarudi Desemba, wakati ambao atatakiwa kuanza kuutumikia mkataba wake na Simba, wakati yupo ndani ya mkataba wa miaka miwili na Yanga.

No comments: