Saturday, August 11, 2012

MBUYU TWITE ACHAFUA HALI YA HEWA MSIMBAZI.

Mbuyu Twite.
 Hali ya wasiwasi imeibuka, kufuatia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuongeza muda wa kufunga usajili kutoka Agosti 10 hadi 15, mwaka huu.
Na inaonekana presha zaidi ipo upande wa Simba SC, ambao wanahofia kuongezwa huko kwa muda kuna lengo la kuwaumiza wao.
Mchezaji ambaye haswa Simba wanahofia kumpoteza ni beki wa kati wa kimataifa wa Rwanda, mwenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Mbuyu Twite iliyemsajili kutoka APR ya Rwanda.

Hiyo inafuatia kuwapo habari kwamba, mtoto wa kigogo mmoja nchini, alikwenda Kigali, Rwanda kwa ajili ya kutaka kuisaidia Yanga kumsajili mchezaji huyo.
Ikumbukwe, wakati Mwenyekiti wa Simba SC, Ismail Aden Rage amekwenda Kigali kuifuata saini ya Twite, alikabiliana na upinzani mkali kutoka kwa mahasimu wao wa jadi, Yanga ambao nao walimtuma Mjumbe wao wa Kamati ya Utendaji, Abdallah Ahmad Bin Kleb kumfuata mchezaji huyo.
Lakini hata hivyo, Rage akafanikiwa kumzidi ujanja Bin Kleb na kuipata saini ya mchezaji huyo. Lakini habari zinasema kwamba, Rage baada ya kuondoka kuwahi Mkutano Mkuu wa mwaka wa klabu yake Dar es Salaam, Bin Kleb aliendelea kumshawishi Mbuyu aghairi kwenda Simba na asaini Yanga.
Inadaiwa ingawa Mbuyu alihoji anawezaje kufanya hivyo wakati amekwishasaini Simba, aliambiwa hilo asiwe na wasiwasi nalo, yeye asaini na ajiunge na Yanga, wao (klabu) watamalizana.
Haieleweki kama Mbuyu amesaini na Yanga pia au la, lakini tu inastaajabisha ameshindwa kujiunga na Simba tangu asaini na ilielezwa angekuwapo kwenye Simba Day Agosti 8, mwaka huu.
Na magazeti mengi ya michezo leo Tanzania yameandika kwamba, Mbuyu Twite amewaambia Simba SC anawarudhishia fedha zao hataki tena kujiunga nao, kwani ameamua kujiunga na Yanga.
Japokuwa Simba leo wanalalamikia Yanga kusaidiwa na mtoto wa kigogo na hapa anazungumziwa Ridhiwani, mtoto wa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, lakini wao pia wakati Maprofesa Philemon Sarungi na Juma Athumani Kapuya walipokuwa wana ‘meno’ kwenye serikali ya Tanzania waliwasaidia mno kuwaliza Yanga.
Katika kuutambua msaada huo, kwenye Simba Day, Simba walimpa tuzo Profesa Sarungi wakati huko nyuma pia wamewahi kumpa tuzo Kapuya pia.
Kapuya alikuwa akiwasaidia Simba kupangua matokeo ya Ligi Kuu ili kuwabeba na hata kubatilisha usajili wa wachezaji, mfano wa Victor Costa, ambaye mwaka 2005 alitakiwa kufungiwa kwa kusaini Simba na Yanga, lakini bwana mkubwa huyo akiwa Waziri wa Wizara yenye dhamana ya michezo, akamuidhinisha Simba.
Mwaka 2001 pia Kapuya aliongeza timu katika Ligi Kuu kwa sababu zake mwenyewe bila kuzingatia Mkataba wa udhamini wa ligi hiyo unasemaje, hali ambayo iliwafanya waliokuwa wadhamini, Safari Lager wakajitoa na kuiponza Simba iliyokuwa bingwa kukosa zawadi.
Kapuya aliwaumiza zaidi Yanga mwaka 1999, kwani wakiwa tayari wamekwishatwaa ubingwa kwa matokeo ya uwanjani, wakiifunga Mtibwa Sugar mabao 2-1 katika mechi ya mwisho Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, enzi hizo bado ukiitwa Taifa, yeye alitengua matokeo na kuipa ubingwa Mtibwa iliyokuwa ya pili. 

No comments: