Wawakilishiwa Afrika
waliokuwa wamebakia katika michuano ya soka ya Olimpiki inayoendelea
jijini London, Uingereza timu za Misri na Senegal zimetolewa katika
hatua robo fainali ya michuano hiyo. Misri
waliyaaga mashindano hayo baada ya kukubali kipigo cha mabao 3-0 kutoka
kwa Japan wakati Senegal wenyewe walifungwa na Mexico mabao 4-2. Kwa
matokeo hayo Japan watakutana na Mexico katika hatua
ya nusu fainali
wakati timu ambayo inapewa nafasi kubwa ya kunyakuwa medali ya dhahabu
kwa mara ya kwanza katika michuano hiyo timu ya Brazil watakutana na
Korea Kusini baada ya kufanikiwa kuifunga Honduras katika hatua ya robo
fainali. Korea
Kusini walitinga katika hatua hiyo baada ya kufanikiwa kuwaondosha
wenyeji Uingereza kwa changamoto ya mikwaju ya penati baada ya timu hizo
kwenda sare ya bao 1-1 katika dakika 120 walizocheza. Nusu
fainali ya michuano hiyo inatarajiwa kufanyika Jumanne ambapo Brazil na
Korea Kusini watakutana katika Uwanja wa Old Traford uliopo jijini
Manchester wakati Mexico na Japan wenyewe watacheza katika Uwanja wa
Wembley jijini London.
No comments:
Post a Comment