Kikosi cha Simba SC.
Michuano ya BancABC SUP8R inayoshirikisha timu nane bora
kutoka Tanzania Bara na Zanzibar inatarajiwa kuendelea leo kwenye miji ya Dar
es Salaam, Moshi, Mwanza na Zanzibar.
Mkurugenzi wa Mashindano wa Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF), Saad Kawemba na viongozi wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) chini ya Rais
wake, Amani Makungu walikutana jana visiwani Zanzibar kuzungumzia maendeleo ya
michuano hiyo.
Viongozi wengine wa ZFA waliohudhuria kikao hicho ni Katibu
Mkuu Kassim Haji Salum na wajumbe saba wa Kamati ya Utendaji.
Katika kundi A Jamhuri itacheza na Zimamoto kwenye Uwanja wa
Amaan, Zanzibar kuanzia saa 2 kamili usiku, wakati Simba itaparurana na Mtende
kwenye Uwanja wa Ushirika, mjini Moshi. Mechi hiyo itaanza saa 10 kamili jioni.
Azam itakuwa mwenyeji wa Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa
Chamazi, Dar es Salaam wakati Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza utakuwa
mwenyeji wa mechi ya Polisi Morogoro na Super Falcon. Mechi hizo zote za kundi
B zitaanza saa 10 kamili jioni.
Hatua hiyo ya makundi itamalizika Agosti 12 mwaka huu kwa
mechi nne. Simba na Zimamoto zitaonyeshana kazi Uwanja wa CCM Kirumba wakati
Jamhuri na Mtende zitacheza kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.
Mechi za kundi B zitakuwa kati ya Super Falcon na Mtibwa
Sugar kwenye Uwanja wa Amaan na Azam dhidi ya Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa
Ushirika.
No comments:
Post a Comment