Usain Bolt.
Mwanariadha nyota wa mbio
fupi, Usain Bolt amesisitiza nia yake ya kutaka kufanya majaribio
katika klabu ya Ligi Kuu nchini Uingereza ya Manchester United. Bolt
raia wa Jamaica mwenye umri wa miaka 25 ambaye ni mwanariadha mwenye
kasi zaidi katika historia ya mbio hizo alifanikiwa kutetea medali yake
ya olimpiki baada ya kufanikiwa kushinda mbio za mita 100 akitumia
sekunde 9.63 na kuvunja rekodi yake
mwenyewe aliyoiweka katika michuano
hiyo mwaka 2008 jijini Beijing. Lakini
Bolt ambaye ni shabiki mkubwa wa klabu ya United ana matarajio kuwa
huko mbele anaweza kubadili mwelekeo na kuamua kucheza soka. Akihojiwa
kuhusiana na hilo Bolt amesema kuwa watu wanafikiri kuwa anatania
kuhusu hilo lakini kama kocha wa United Sir Alex Ferguson akimuita kwa
ajili ya majaribio basi hatasita kufanya hivyo kwani anaupenda mchezo wa
soka. Bolt
amesema kuwa asingekubali changamoto hiyo kama hangejiona kama anaweza
lakini anajiamini kwamba ni mchezaji aliyekamilika na anajua anaweza
kuleta mabadiliko. Nyota
huyo ambaye anatarajiwa kutetea medali yake katika mbio za mita 200
Agosti 9 mwaka huu, aliongeza kuwa bado yuko jijini London kwa siku
kadhaa hivyo kama Ferguson atamhitaji anajua mahali pa kumtafuta.
No comments:
Post a Comment