Mkuu wa
mkoa wa Katavi, Dr Rajabu Rutengwe amewataka wawekezaji wanaokwenda kuwekeza
katika sekta ya madini katika mkoa wa Katavi wawasiliane na ofisi za serikali
mkoani humo kabla ya kuingia katika mikataba ya uendeshaji wa shughuli za
uzalishaji katika maeneo husika
Mwandishi
wa habari hii kutoka Katavi Willy Sumia anaripoti kuwa wito huo umetolewa na
mkuu kufuatia utapeli waliofanyiwa wawekezaji wa kutoka nchi ya China na kampuni
yao ya Red Ore Mining Co. Ltd ya DSM na kupelekwa eneo la pori la akiba la Luafi
mpakani na hifadhi ya Taifa ya Katavi kwa ajili ya kuendesha shughuli za
uchimbaji wa madini ya chuma na shaba.
Taarifa
zinasema kuwa kampuni hiyo yenye makao yake jijini DSM inayoendeshwa na Raia wa
nchi ya China ilianza shughuli katika eneo hilo katika kipindi cha mwezi mmoja
uliopita hadi jana walipofika askari wa wanyamapori wa Pori la akiba la Rukwa /
Lukwati/ Luafi na hifadhi ya Taifa ya Katavi kuwaamuru waondoke katika eneo hilo
kwakuwa ni eneo lilitengwa kwa ajili ya uhifadhi wa mazingira na ustawi wa
wanyama pori.
Askari
hao walipozungumza na waandishi wa habari walisema kuwa awali walipowakuta raia
hao wa China waliweza kuwahoji na kubaini kuwa walikuwa wameingizwa eneo hilo
kimakosa na ofisi ya hifadhi hiyo iliwaandikia barua yenye Kumb Namba
RLLGR/LGR.1/72/14 ya tarehe 06/06/2012 iliyokuwa akiwapa amri ya kuondoka eneo
ndani ya siku saba tangu tarehe ya barua hiyo lakini hawakuweza kutekeleza agizo
hilo
Askari
hao wa wanyamapori walisema kutokana na kushindwa kutii agizo hilo waliamua
kufika eneo husika kuwachukua viongozi wa kampuni hadi ofisi ya Mkuu wa mkoa kwa
maamuzi zaidi kwani walibaini kuwa walipewa taarifa za uongo na mtu aliyewauzia
hilo eneo kwani hilo eneo na eneo lisilotakiwa kufanyiwa shughuli yoyote
ile
Walisema
hata barua walizojibiwa na Katibu Mkuu wa wizara ya Maliasili na Utalii yenye
kumbukumbu namba HB 178/286/01/102 iliyosainiwa na ndugu J. Muya kwa niaba ya
Katibu mkuu wa wizara hiyo ya tarehe 20/06/2012 pamoja na ile iliyotoka kwa
wakala wa misitu Tanzania (TFS) yenye kumbukumbu namba TFSC.166/286/01/29 ya
tarehe 25 Juni, 2012 ikieleza kuwa eneo hilo waliloomba kwa barua siyo eneo
linaloruhusiwa kwa kufanya shughli yoyote ya kibinadamu isipokuwa kwa utafiti wa
mafuta, gesi au madini ya uraniamu tu
Akizungumza
na waandishi wa habari mara baada ya kikao na Wachina wamiliki wa Kampuni ya
RedOre Mining Co. Ltd, mkuu wa mkoa wa Katavi, Dr Rajabu Rutengwe alisema kuwa
katika mazungumzo na wawekezaji hao alibaini kuwa walitapeliwa na mtu
aliyewauzia eneo hilo baada ya kuona kuwa eneo hilo haliruhusiwi kwa shuguli
yoyote.
Alisema
kutokana na hali iliyojitokeza inabidi sheria ichukue mkondo wake na huku
wawekezaji hao wakiwa nje ya hifadhi kwani tayari eneo hilo limeshaharibiwa na
kuingiza hasara kubwa Taifa hivyo ili kuepusha malalamiko ya kuwa wageni hao
wameonewa na Watanzania hivyo mahakama ndiyo itakayoamua nani kakosea, wapi na
namna gani kakosea ili kulinda utawala bora.
Akizungumzia
juu ya aliyewatapeli wawekezaji hao mkuu wa mkoa alisema wao ndio wanamfahamu
aliyewauzia na wanafahamu watampata wapi hivyo ni jukumu la wawekezaji kumtafuta
wamuawajibishe kwa kuwatapeli ambapo mkuu huyo wa mkoa alitoa ushauri kwa
wawekezaji wengine wasiingie mkataba na mmiliki yeyote wa ardhi katika mkoa wa
Katavi bila kuwasiliana na Halmashauri au ofisi ya madini ya kanda ya Magharibi
iliyoko mjini Mpanda kwa ushauri na msaada wa taarifa za eneo husika
No comments:
Post a Comment