Mhe. Dk. Ali Mohamed.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein(pichani), ameiagiza
Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo
kuandaa utaratibu wa kupata fedha ndani ya wiki moja kwa ajili ya
kununua meli kubwa mpya ya abiria wapatao 1000 na yenye uwezo wa
kuchukua mizigo ya tani 100.
Dk. Shein ametoa agizo hilo leo
wakati alipokuwa na mazungumzo na uongozi wa Shirika la Meli pamoja na
Wajumbe wa Bodi ya Shirika hilo ambapo pia kikao hicho kilihudhuriwa na
uongozi wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano na Wizara ya Nchi Afisi
ya Rais Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo.
Katika kikao hicho maalum Dk. Shein
ameiagiza Wizara hiyo kutafuta fedha hizo kutokana na vianzio vya ndani
au nje ya nchi ama kutokana na taasisi zinazohusiana na mambo ya
fedha.
Alieleza kuwa katika kipindi
kisichozidi miezi miwili ujumbe maalum uende kwa Kampuni
zinazotengeneza meli nchini Korea Kusini, China au Japan kwa ajili ya
kuwasilisha fedha za utangulizi kwa ajili ya ujenzi wa meli hiyo.
Mapema uongozi wa Shirika la Meli,
ulimueleza Dk. Shein kuwa kwa kawaida ujenzi wa meli yenye ukubwa huo,
huchukua mwaka mmoja kukamilika.
Kikao hicho ambacho kilikuwa na
lengo la kuangalia mwelekeo na Mipango ya Shirika la Meli pia,
kilijadili hali halisi ya meli za Shirika la Meli na baadae kujadili
masuala ya ununuzi wa meli mpya itokayowaondoshea usumbufu wa usafiri wa
baharini wananchi wanaosafiri kati ya Unguja, Pemba na Tanzania Bara.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar.
No comments:
Post a Comment