Wadau
wa Sanaa wamehoji uhalali wa wasanii wa filamu kutumia kiingereza
kwenye majina ya filamu zao huku wakishangazwa na kazi hizo kubeba
maudhui ya kizungu zaidi.
Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti,
Mafunzo na Habari kutoka Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Godfrey
Lebejo akisisitiza jambo wakati akihitimisha programu ya Jukwaa la Sanaa
wiki hii. Kulia kwake ni Kaimu Mratibu wa Jukwaa hilo Agnes Kimwaga.
Wakizungumza wiki hii kwa nyakati tofauti kwenye programu ya Jukwaa
la Sanaa, wadau hao walishangazwa kitendo cha filamu hizo kutumia majina
ya kizungu wakati hapa kwetu kuna filamu nyingi kutoka nje zinazotumia
lugha za kihindi, kichina, kifaransa na zinafanya vizuri.
“Hoja kwamba, wanatumia majina ya kiingereza ili kuteka soko la
kimataifa ni ya kitoto, mbona hapa kwetu kuna filamu nyingi za kihindi
na kichina zinanunuliwa kwa wingi? Hapa kuna udhaifu katika kutengeneza
filamu zenye ubora tujikite huko”alisema Mzee Nkwama Bhallanga.
Kwa mujibu wa wadau wengi waliozungumza, filamu ni taaluma
inayozungumza kwa kutumia picha na vitendo zaidi hivyo haihitaji
mtazamaji kufahamu lugha iliyotumiwa ili afahamu maudhui na ujumbe
unaowasilishwa na kazi husika ya filamu.
“Maneno kwenye filamu si muhimu sana, kinachozungumza ni matendo na
picha zaidi, ndiyo maana kuna watu wanaangalia picha za Kikorea na
wanaburudika na kuelewa kinachoendelea” alisema Godfrey Lebejo ambaye ni
Murugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na habari, BASATA.
Aliongeza kuwa, kinachoitesa tasnia ya filamu kwa sasa ni kukosekana
kwa weledi na uhalisia wa tamaduni zetu kunakosababishwa na wimbi kubwa
la watu kujiingiza kwenye filamu ili kufanikisha mambo yao yaliyo nje ya
maadili na utamaduni wetu.
“Inawezekana vipi utengeneze filamu ambayo baba, mama na watoto
hawawezi kukaa pamoja kuitazama? Tufike mahali tuseme mambo haya ya
kipuuzi basi kwenye filamu zetu” alionya Lebejo.
Awali akiwasilisha mada kuhusu Filamu, wasanii na haja ya
kujiendeleza kielimu, Msanii wa filamu Emmanuel Myamba maarufu kam
Pastor Myamba alisema kuwa, tasnia ya filamu inakosa weledi hivyo
kuhitaji mabadiliko.
“Ni wazi ukiangalia filamu zetu zinakosa weledi katika uandishi wa
miswada, uongozaji, uhariri na hata uumbaji wa wahusika. Lazima tukubali
udhaifu huu turekebishe” alisema Myamba ambaye kwa sasa amefungua kituo
cha mafunzo ya filamu kiitwacho Tanzania Film Training Centre (TFTC)
kilichoko Ubungo.
No comments:
Post a Comment