
Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi wa
Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw. Morrice Oyuke akiongea na waandishi wa
habari leo jijini Dar es Salaam kuelezea hali ya Ukuaji wa Pato la
Taifa kwa 7.1% katika kipindi cha robo mwaka 2012.
Ofisi ya Taifa ya
Takwimu (NBS) imetoa taarifa ya hali ya uchumi nchini na kufafanua kuwa
pato la taifa la Tanzania limekua kwa asilimia 7.1 katika kipindi cha
robo ya mwaka 2012 ikilinganishwa na asilimia 6.1 za mwaka jana.
Ukuaji huo wa asilimia
7.1 unatokana na ongezeko la uzalishaji katika shughuli mbalimbali za
kiuchumi zikiwemo za kilimo, Uvuvi, Viwanda, Ujenzi na zile za utoaji
wa huduma mbalimbali za jamii.
Akitoa taarifa hiyo
jana jijini Dar es salaam Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi wa Ofisi ya
Taifa ya Takwimu Bw. Morrice Oyuke amesema kuwa lengo la utoaji wa
taarifa hizo kwa vipindi vifupi vya vya robo mwaka unalenga kuwapatia
wadau wa Takwimu za Pato la Taifa uwezo wa kutathmini mabadiliko ya
ukuaji wa uchumi nchini.
Amesema kuwa jumla ya
thamani ya pato la Taifa katika kipindi cha robo ya mwaka 2012 ni
shilingi 4,220,535 milioni ikilinganishwa na kiasi cha shilingi milioni
3,940,261 za mwaka 2011.
Amefafanua kuwa ukuaji
wa shughuli uzalishaji katika shughuli za kilimo nchini ulifikia
asilimia 1.4 katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2012
zikilinganishwa na asilimia 1.2 katika kipindi hicho kwa mwaka 2011
kutokana na upatikanaji wa mvua za kutosha nchini katika mikoa
inayozalisha mazao kwa wingi.
Amesema ukuaji katika
shughuli za uvuvi ulikua asilimia 2.6 katika robo ya kwanza ya mwaka
2012 huku shughuli za uchumi katika sekta ya viwanda na Ujenzi ambayo
inahusisha uchimbaji wa madini na kokoto ikikua kwa asilimia 14.3
ikilinganishwa na 0.8% za mwaka 2011.
Bw. Oyuke ameongeza
kuwa ongezeko hilo la uzalishaji wa madini ya dhahabu linatokana na
uzalishaji wa wa madini ya dhahabu kutoka kilo 8,140 kwa mwaka 2011
hadi kufikia kilo 16,736 kwa mwaka 2012.
Pia amebainisha kuwa
shughuli za utoaji wa huduma za biashara za jumla na rejareja,
ukarabati wa magari na pikipiki na vifaa vingine vya majumbani katika
kipindi hicho zilifikia asilimia 9.0 huku shughuli za upangishaji
nyumba na biashara zikiwa 8.2 %, uchukuzi na mawasiliano 16.4%, hoteli
na migahawa 3.8%, Benki asilimia 15 shughuli za uendeshaji serikali
6.4%, Elimu 6.1% na utoaji wa huduma za Afya nchini zikikua kwa kasi ya
asilimia 5.1.
No comments:
Post a Comment