Wednesday, August 8, 2012

SIMBA DAY MAMBO BABU KUBWA TAIFA LEO.

Nahodha wa Simba, Juma Kaseja akiwa amebebwa juu na wenzake baada ya kutwaa Kombe la Urafiki.
 Kikosi kizima cha wachezaji wa Simba SC, leo kinatarajiwa kutambulishwa rasmi mbele ya maelfu ya mashabiki wake, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati wa tamasha maalum la kila mwaka la klabu hiyo, Simba Day.
Tamasha hilo, litakalotanguliwa na burudani ya muziki ya bendi ya Msondo Ngoma, litahitimishwa kwa mchezo wa kirafiki kati ya Nairobi City Stars na Simba SC.

Kama ilivyo ada ya tamasha hilo, watatambulishwa wachezaji wote waliosajiliwa Simba kwa ajili ya msimu ujao na hapo ndipo panatarajiwa kuwa na msisimko zaidi. Wachezaji wote wa Simba tayari wapo Dar es Salaam, akiwemo Emmanuel Okwi, wakati Mbuyu Twite aliyesajiliwa kutoka APR ya Rwanda anatarajiwa kuwasili mapema leo na atakuwapo pia Taifa.
Kuelekea tamasha hili, Simba iliendesha Wiki ya Simba na Jamii, wakitembelea kituo cha watoto yatima cha Maungu Orphanage Center, kilichopo Kinondoni Mkwajuni, Hospitali ya Mwananyamala, Dar es Salaam na baada ya tamasha la leo, Simba watatembelea shule ya msingi Mgulani, ambayo mastaa wengine kibao bongo kama Rashid ‘Snake Boy’ Matumla wamesoma ili kuhamasisha michezo mashuleni.
Wiki ya Simba na Jamii itahitimishwa kwa ziara ya kiwanda cha Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kilichopo Ilala, Dar es Salaam, Agosti 10.
TBL ndio wadhamini wakuu wa Simba SC, kupitia bia yao ya Kilimanjaro Premium Lager, ambayo pia ndio imedhamini Wiki nzima ya Simba na Jamii, kuanzia kwenye Mkutano Mkuu wa mwaka wa klabu hiyo, Jumapili Bwalo la Maofisa wa jeshi la Polisi, Oysterbay, Dar es Salaam, 
Katika kipindi cha zaidi ya miaka 70 ya kuwepo kwake, Simba inajivunia kuwa klabu yenye rekodi nzuri zaidi ya kibalozi, ikiwa klabu pekee Tanzania kucheza fainali ya michuano ya Afrika, Kombe la CAF mwaka 1993, ambako ilifungwa na Stellah Abidjan 2-0, klabu pekee kucheza Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, mwaka 1974 ikitolewa na Mehallal El Kubra kwa penalti.
Simba pia ndio klabu kwa ujumla, iliyotwaa mara nyingi zaidi ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, mara sita katika miaka ya 1974, 1991, 1992, 1995, 1996 na 2002. 
Na hata katika historia ya utani wake wa jadi na wapinzani wao, Yanga- Simba wanajivunia kushinda mabao mengi zaidi katika mechi moja, 6-0 mwaka 1977. Yanga waliwahi kuifunga Simba 5-0 mwaka 1968 na Simba wakazilipa mwaka jana.

No comments: