Tuesday, August 7, 2012

BOLT ATAMANI KUFANYA MAJARIBIO MAN UNITED.

Usain Bolt.
Mwanariadha nyota wa mbio fupi, Usain Bolt amesisitiza nia yake ya kutaka kufanya majaribio katika klabu ya Ligi Kuu nchini Uingereza ya Manchester United. Bolt raia wa Jamaica mwenye umri wa miaka 25 ambaye ni mwanariadha mwenye kasi zaidi katika historia ya mbio hizo alifanikiwa kutetea medali yake ya olimpiki baada ya kufanikiwa kushinda mbio za mita 100 akitumia sekunde 9.63 na kuvunja rekodi yake
mwenyewe aliyoiweka katika michuano hiyo mwaka 2008 jijini Beijing. Lakini Bolt ambaye ni shabiki mkubwa wa klabu ya United ana matarajio kuwa huko mbele anaweza kubadili mwelekeo na kuamua kucheza soka. Akihojiwa kuhusiana na hilo Bolt amesema kuwa watu wanafikiri kuwa anatania kuhusu hilo lakini kama kocha wa United Sir Alex Ferguson akimuita kwa ajili ya majaribio basi hatasita kufanya hivyo kwani anaupenda mchezo wa soka. Bolt amesema kuwa asingekubali changamoto hiyo kama hangejiona kama anaweza lakini anajiamini kwamba ni mchezaji aliyekamilika na anajua anaweza kuleta mabadiliko. Nyota huyo ambaye anatarajiwa kutetea medali yake katika mbio za mita 200 Agosti 9 mwaka huu, aliongeza kuwa bado yuko jijini London kwa siku kadhaa hivyo kama Ferguson atamhitaji anajua mahali pa kumtafuta.

No comments: